NDEGE YA MGOMBEA MWENZA WA TRUMP YAPATA AJALI
Mgombea mwenza wa chama cha Republican katika kinyang'anyiro cha urais nchini Marekani Mike Pence amenusurika baada ya ndege iliyombeba kuteleza uwanja wa ndege.
Ndege hiyo iliteleza na kuvuka barabara inayotumiwa na ndege kupaa na kutua katika uwanja wa LaGuardia jijini New York.
Gavana huyo wa Indiana amewaambia wanahabari kwamba yuko salama baada ya kisa hicho.
Hakuna aliyejeruhiwa.
- Trump v Clinton: Nani anaongoza?
- Obama: Trump hafai kuwa rais
- Trump: Kura zinaibiwa vituoni Marekani
Bw Pence na abiria wengine takriban 30 waliokolewa kupitia mlango wa dharura wa ndege upande wa nyuma.
Alikuwa anatoka mkutano wa kampeni Fort Dodge, Iowa.
Uwanja wa ndege wa LaGuardia kwa muda usiojulikana, maafisa wamesema.
Rubani anadaiwa kukanyaga breki na abiria wanasema walinusa harufu ya raba ikiungua.
Kanda za video za runinga zimemuonesha Bw Pence baadaye akiwa amesimama kwenye mvua karbu na magari ya huduma za dharura, akizungumza na baadhi ya maafisa.
Baadaye aliandika kwenye Twitter: "Nashukuru sana kwamba kila mtu aliyekuwa kwenye ndege yetu yuko salama. Nashukuru maafisa wa dharura na wote waliotuombea. Tutarejea kwenye kampeni kesho!"
Amesema matope yaliruka na kujaa kwenye kioo cha sehemu ya mbele ya ndege.
Mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump alimpigia simu Bw Pence kumjulia hali baada ya kisa hicho, maafisa wa kampeni wamesema.
Msemaji wa Trumo Stephanie Grisham alisema mgombea huyo alikuwa kwenye msafara wa kampeni akielekea Geneva, Ohio.
Bw Trump alizungumzia ajali hiyo kwenye mkutano wake wa kampeni baadaye akisema: "Mnajua, kulitokea ajali kubwa ya ndege.
"Ndege imeteleza kutoka barabara uwanja wa ndege na ilikaribia sana kuwa mbaya, kuwa mbaya sana, nimezungumza na Mike sasa hivi na yuko salama. Alitoka. Kila mtu yuko salama."
Bw Pence aliahirisha hafla ya kuchangisha pesa ambayo ilifaa kuandaliwa katika jumba la Trump Tower eneo la Manhattan, na akaelekea moja kwa moja hadi hotelini.
Haijakuwa wiki njema kwa gavana huyo wa Indiana.
Jumatano, alitangaza kwenye Twitter kwamba mbwa wake kwa jina Maverick, alikuwa amefariki akiwa na miaka 13.
No comments:
Post a Comment