HABARI, BIASHARA, MUSIC, SIASA, MICHEZO,

Sunday, 27 November 2016

ALICHO KISEMA KATIBU MKUU WA BMT BAADA YA KUTOELEWEKA KAULI YAKE YA MWANZO JUU YA UENDESHWAJI MPYA WA VILABU VYA SIMBA NA YANGA


KUMBE Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja, hakueleweka vizuri wakati alipozungumzia suala la mabadiliko ya kiuendeshaji katika klabu za Simba na Yanga na sasa ameamua kuweka mambo sawa.
Akiwa kwenye mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya  Lord Baden Powel wilayani Bagamoyo, Pwani, Kiganja alisema hakuna sehemu Serikali imezuia mabadiliko katika klabu kongwe nchini za Simba na Yanga na kilichotokea ni yeye kunukuliwa vibaya tu.
Kiganja alisema ambacho alisema yeye ni kuwa ni lazima klabu hizo mbili kongwe na zenye mashabiki wengi zaidi nchini pamoja na nyingine zinazotaka, zifuate kanuni na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
“Huwezi kuyazuia mabadiliko kwa namna yoyote ile na ndiyo maana hata  baada ya kupata Uhuru wa Tanganyika na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu  Julius Nyerere, alipounda Tanzania bado wananchi walihitaji mabadiliko.



“Hivyo ieleweke wazi kwamba Serikali haijazuia mabadiliko katika michezo, tunachotaka utaratibu ufuatwe lazima kila kitu kiwekwe kwenye ‘proper document,” alisema.
Kiganja alisema klabu inapotaka kufanya mabadiliko inapaswa kuunda sera ambayo baadaye itakuwa sheria na kisha kuingizwa katika Katiba.
Katika hatua nyingine, Kiganja alizishangaa klabu kubwa nchini kugombea kusajili wachezaji wa kigeni badala ya kusaka vipaji shuleni ambako vimejaa na kukuza michezo kwa ujumla.
Alisema kitendo cha klabu kusajili wachezaji wengi kutoka nje ya Tanzania,  kunalitia taifa hasara kubwa kwa kukosa wachezaji wa kuunda timu ya Taifa.

Kiganja amekuwa kwenye vichwa vya habari katika siku za hivi karibuni kutokana na kauli ambazo amekuwa akitoa kuhusiana na mabadiliko ya Simba na Yanga, huku mara ya mwisho akizungumzia Mkutano Mkuu wa Simba, kitendo kilichosababisha Msemaji wa klabu hiyo ya Msimbazi kuibuka na kumshangaa katibu huyo.

No comments:

Post a Comment