CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekuja na mkakati mpya
wa mikutano ya ndani iliyopewa jina la amsha amsha itakayodumu kwa siku
40 nchi nzima.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata Dar es Salaam jana na
kuthibitishwa na ofisa mmoja wa ngazi za juu wa chama hicho, zinasema
viongozi wa Kamati Kuu na wabunge wote wa chama hicho watakutana mkoani
Morogoro kuanzia kesho.
“Kweli kikao hiki kipo, viongozi wetu wa Kamati Kuu na wabunge wote
wa chama tunakutana Morogoro kupeana majukumu ya chama chetu,” alisema
ofisa huyo.
Alisema kikao hicho kitakachoongozwa na Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe, kitakuwa na ajenda moja kubwa ya kupanga mikakati ya
mikutano ya ndani kuimarisha chama hicho kuanzia ngazi ya kitongoji,
kata, kijiji, wilaya na mkoa.
“Mbowe ataongoza kikao hiki kama mwenyekiti wetu, lengo letu
kuwafikia wafuasi wetu kuanzia ngazi za chini, maana huko ndiko chama
kilipo… tunafanya hivi kwa sababu mikutano hii imeruhusishwa na mamlaka
husika,” alisema ofisa huyo.
Alisema katika kikao hicho, wanatarajia kuunda timu tatu ambazo zitazunguka kila jimbo la uchaguzi na kuweka mikakati yao.
“Tutaunda timu tatu ambazo zitapewa majukumu ya chama na kuzunguka
nchi nzima, siwezi kukwambia nani atakuwa wapi, tusubiri kidogo
itajulikana kuanzia kesho,” alisema ofisa huyo.
Hatua hii imekuja baada ya miezi kadhaa tangu chama hicho kutangaza
kufanya maandamano na mikutano nchi nzima – Operesheni Ukuta ambayo
ilisababisha Jeshi la Polisi kuipiga marufuku.
Operesheni hiyo iliyotarajiwa kufanyika Septemba mosi, mwaka huu,
ambayo pamoja na mambo mengine ililenga kuishtaki Serikali ya Rais Dk.
John Magufuli kwa umma kutokana na aina ya uongozi wake, iliibua mvutano
mkali kati ya Chadema na Jeshi la Polisi.
Jeshi hilo lilitoa onyo kali kwa mtu yeyote ambaye angeandamana, huku
kwa mara ya kwanza Watanzania wakishuhudia askari kila mkoa wakifanya
mazoezi makali.
Baada ya mvutano huo, Mbowe alitangaza kuahirisha operesheni hiyo
hadi Oktoba mosi, mwaka huu, kutoa nafasi kwa Rais Magufuli kufanya
mazungumzo na viongozi wa dini kwa ajili ya upatanisho
No comments:
Post a Comment