HABARI, BIASHARA, MUSIC, SIASA, MICHEZO,

Thursday, 3 November 2016

LEMBELI AMFUNGUKIA MAGUFULI KUHUSU MAJANGI! AWATAJA KWA MAJINA


VITA dhidi ya ujangili nchini imezidi kupata nguvu mpya baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira katika Bunge la 10, James Lembeli, kumuonyesha Rais John Magufuli mahala pa kuwanasa vigogo wa biashara hiyo haramu.


Akizungumza  jana, Lembeli alisema vita dhidi ya ujangili iliyopata msukumo mpya kutokana na agizo la Rais Magufuli alilolitoa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii mwishoni mwa wiki, itapata mafanikio zaidi endapo orodha ya ‘majangili papa’ iliyomo kwenye ripoti ya ‘Operesheni Tokomeza’ itatua kwa Rais Magufuli na kufanyiwa kazi.

Akizungumzia maagizo aliyoyatoa Rais Magufuli, Lembeli alisema ni jambo jema, na kwamba kufanikiwa kwake kutatokana na utekelezaji wa ripoti ya ‘Operesheni Tokomeza’, aliyodai kwamba ilitaja mtandao wa vigogo muhimu pamoja na wafanyabiashara.

Juammosi iliyopita, Rais Magufuli alifanya ziara ya ghafla katika jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii la Mpingo House jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo kadhaa kuhusiana na vita dhidi ya ujangili. Siku hiyo Rais alimteua Jenerali mstaafu George Waitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa). 

Aidha, katika ziara yake hiyo, Rais Magufuli alisisitiza kuwa yuko nyuma ya vita dhidi ya ujangili na hivyo (operesheni) isimuache yeyote, kwa maana ya kuwakamata wahusika wa ujangili bila kujali cheo cha mtu, umri, jina, kabila, rangi wala dini yake. 

Alisema hayo baada ya kuona meno ya tembo 50 yaliyokamatwa, kuwaona watuhumiwa na pia kuelekeza kuwa anayo taarifa juu ya vikwazo mbalimbali kuhusiana na udhibiti wa vitendo hivyo.

UFAFANUZI KUHUSU ‘MAJANGILI PAPA’

Lembeli aliyekuwa akizungumza  baada ya kuulizwa maoni yake kuhusiana na kasi mpya katika vita dhidi ya ujangili, alisema wahusika wa vitendo hivyo ni baadhi ya vigogo waliokuwapo na waliopo hadi sasa serikalini.

Akifafanu, Lembeli alisema ni vigogo hao wasio waaminifu ndani ya Serikali ndiyo wanaolea biashara hiyo kwa namna mbalimbali, ikiwamo ya kuvujisha taarifa muhimu ambazo ndizo huwawezesha majangili kutekeleza uhalifu huo bila ya kuguswa na mkono wa dola.

Lembeli ambaye alikuwa Mbunge wa Kahama kabla ya kupoteza nafasi hiyo baada ya kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujaribu kutetea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema anampongeza Rais Magufuli kwa hatua yake ya kutoa maelekezo muhimu katika vita dhidi ya ujangili.

Alisema anampongeza na kumuunga mkono kwa asilimia 100 Rais Magufuli, akidai kwamba anachokifanya sasa ndicho hasa kilichoelezwa kwenye ripoti ya ‘Operesheni Tokomeza’.

“Wakati ule, badala ya Serikali ya Awamu ya Nne kuifanyia kazi ripoti ile, wakaanza kuwashutumu watu kwamba siyo wana CCM,” alisema Lembeli.

Akitoa mfano, Lembeli alidai kuwa ndani ya ripoti hiyo, yumo kigogo mmoja wa polisi alisaidia kujaribu kutorosha meno ya tembo yaliyokuwa yamewekwa kwenye gari lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yake.

“Huyo kigogo mpaka leo yupo. Kama Magufuli ataitumia vizuri ripoti ya Operesheni Tokomeza, vigogo hao wa ujangili watapatikana… na akitaka tumsaidie tutafanya hivyo. Asiwafuate wafanyabiashara peke yao. Ni kwa sababu wafanyabiashara hawa wanaongozwa na baadhi ya vigogo wa serikali,” alisema na kuongeza.

“Hakuna mfanyabiashara wa meno ya tembo anayeweza kufanikiwa kwenye hiyo biashara bila kushirikiana na watendaji wa Serikali. Wao ndiyo wanawapa mbinu zote.” 

No comments:

Post a Comment