Friday, 4 November 2016
UPINZANI WA MUUNGA MKONO JPM
WABUNGE wa upinzani wamemwelezea Rais John Magufuli kuwa ni mtu mwenye ujasiri wa pekee ambao watu wengi hawana, kwani amefanikiwa kurejesha nidhamu na kupambana na rushwa.
Pia wamemwelezea Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa ni kiongozi aliyeisaidia nchi kuendelea mbele katika eneo la uwekezaji na kutoa uhuru wa Watanzania kutoa maoni.
Wakichangia mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/2018 na mwongozo wa bajeti ya Serikali wa mwaka 2017/2018 juzi, bungeni mjini hapa, wabunge hao kwa nyakati tofauti walisema pamoja na kwamba si mambo yote anafanya vizuri, lakini Rais ni jasiri na ameweza kushughulikia rushwa.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), alisema mtu atakuwa wa ajabu akikataa kutambua dhamira ya Rais ya kurejesha nidhamu na kupambana na rushwa. Alisema Rais amerejesha nidhamu, pia ameonesha dhamira njema katika kupambana na rushwa nchini lakini akataka anapokosea kwa kuwa naye ni binadamu, aambiwe.
“Rais anapofanya vizuri, aambiwe na anapokosea, aambiwe, kama nyie (akielekeza upande wanakokaa wabunge wa CCM na mawaziri) hamtamwambia, sisi tutasema,” alisema Msigwa.
Msigwa aligusa na kusifu utendaji kazi wa marais waliopita, kuanzia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere hadi Jakaya Kikwete, akisema walifanya mambo mazuri na Magufuli pia.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa CCM walishangazwa kwa sifa hizo hasa kwa Rais Kikwete ambaye wapinzani walimbeza enzi akiwa madarakani na kudai nchi imemshinda. Mbunge wa Viti Maalum, Felista Bura (CCM) alisema wapinzani walikuwa wakisema Kikwete anachekacheka, hawezi kuongoza nchini.
“Walikuwa wanasema JK (Jakaya Kikwete) anachekacheka, leo wanamsifu?” alishangazwa Bura. Mbunge wa Jang’ombe, Ali Hassan King (CCM) alisema ikiwa sasa wapinzani wanaona Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Kikwete walikuwa wazuri, hata Magufuli watampenda tu na kumuona mzuri siku zijazo.
Nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge wengine wa upinzani walizungumza na gazeti hili na kuunga mkono juhudi za wazi za kuimarisha nidhamu kwa watumishi wa umma na kupambana na ufisadi zinazofanywa na Rais Magufuli. Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), alisema, “Ukweli lazima niseme yapo maeneo ambayo Rais amefanya vizuri na mengine bado”.
Sakaya alisema eneo la kuzuia mianya ya rushwa kwa kusimamia mapato, kubana fedha watu ambazo awali zilikuwa zikichezewa ovyo na kurejesha nidhamu ya kazi iliyopotea muda mrefu nchini, inapaswa ipongezwe.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF), alisema utendaji kazi wa rais ni mzuri hasa eneo la kurejesha maadili na nidhamu katika kazi hasa kwa watumishi wa umma.
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment