Thursday, 3 November 2016
YAJUE MAKOSA MAKUBWA ALIO YAFANYA RAIS OBAMA WA MAREKANI KATIKA UONGOZI WAKE
Tangu utawala wa Rais Franklin Delano Roosevelt, marais wa Marekani wamekuwa wakipimwa kufuatia mafanikio wanayokuwa wameyafikia katika kipindi cha siku 100 za kwanza za urais wao.
Lakini sasa, Rais Barack Obama akiwa katika maandalizi ya kumaliza muda wake wa utawala, Mtandao wa ‘Yahoo’, umetoa taarifa zinazoakisi utawala wa rais huyo kwa kutazama mafanikio na magumu aliyopitia.
Kimsingi rais huyu ataondoka madarakani katikati mwa mwezi Januari mwakani lakini ifahamike kwamba, kuwa Rais wa Marekani kunatoa fursa na madaraka makubwa kwa rais wa nchi hiyo.
Kuna kipindi kingine madaraka hayo hutoa mwanya wa kufanya makosa makubwa. Kwa kiongozi mwenye nafasi hiyo kitendo cha kufanya makosa yawe makubwa au madogo yanaweza kutoa madhara ya kusikitisha wakati wote.
Na mara nyingi makosa hayo hubaki katika historia au kuandikwa mara kwa mara katika vyombo vya habari.
Japokuwa Obama anaondoka madarakani, kuchambua makosa yake makubwa na mafunzo tunayoweza kuyapata kutokana na masuala aliyoyafanya ni jambo muhimu sana sasa hasa kipindi hiki ambacho rais mpya anatarajiwa kuja huku Marekani na dunia ikikabiliwa na vita dhidi ya kundi la ‘Islamic State’, au maarufu kama ISIS.
Wachambuzi wa utawala wa Obama wale wa mrengo wa kushoto au kulia wengi wana maoni tofauti kuhusu makosa makubwa aliyoyafanya Obama katika kipindi cha utawala wake.
Lakini pia Rais Obama mwenyewe amejifanyia tathmini mara kadhaa na tathmini ya karibuni kabisa ni ile aliyoitoa kupitia mahojiano na kituo cha televisheni cha Fox News mwezi Aprili mwaka huu.
Akiwa na mwendesha kipindi hicho Chris Wallace, Obama aliulizwa kuhusu makosa makubwa aliyofanya wakati wa utawala wake na akajibu: “nadhani ni kushindwa kujipanga vema kuhusu nini kingefuata baada ya kuivamia Libya.”
Julai, 2012 akiwa katika kampeni za uchaguzi wake wa pili aliulizwa na Televisheni ya CBS kuhusu mambo aliyoshindwa katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi naye akasema: “kosa langu kubwa katika kipindi changu cha kwanza lilikuwa kuwaza kwamba kazi hii inahitaji zaidi kupata sera sahihi.
Ni kweli hilo ni jambo muhimu. Lakini kazi hii pia inakuhitaji uwaambie Wamarekani taarifa zinazowapa matumaini na kuwaunganisha zaidi. Taarifa zinazoonesha malengo na matarajio ya kufanikiwa hata katika vipindi vigumu.”
Obama aliakisi pia hali ya wasiwasi uliojengeka katika kipindi cha kampeni mwaka 2008 ambapo wengi walisema alikuwa anatoa hotuba nzuri lakini swali likabaki je, atamudu kazi ya urais? Hadi kufikia mwaka 2012 wengi wakabadilika baada ya kuona kuwa kuna mambo mengi mazuri ameyasimamia vema na hivyo akawa na kazi tu ya kuwaelezea Wamarekani njia anayotaka kuwapeleka katika kipindi cha pili.
Desemba, 2013 kitendo cha taarifa za wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma za bima ya afya zilizokuwa kwenye mtandao zilipokabiliwa na mushkeli wa kuingiliwa kimawasiliano kilimfanya kujutia mkakati wake wa kwanza alioamini ungeweza kuleta mageuzi makubwa kwa watumiaji wa huduma za afya nchini Marekani.
Obama aliamini kuwa wataalam wake aliokuwa nao wa Teknolojia ya Mawasiliano wasingeweza kukumbwa na zahama hilo la mtadao wao kuingiliwa hali iliyoleta sintofahamu kwa wanachi wengi wa Marekani na yeye kama Rais ikambidi kuomba radhi hadharani.
“Kwa kuwa mimi ndiye niliye na mamlaka kuhusu hili, naweza kutamka kuwa tulifanya makosa. Msidhani kuwa sijifanyii tathmini ya mambo ninayoyafanya.
Nawapa taarifa tu kuwa natumia muda mwingi sana kujitathmini kuliko wengi wenu mnavyofanya kila siku,” Obama alisema akiwajibu waandishi wa habari Jonathan Karl wa ABC na Ed Henry wa Fox News.
Kwa miaka mwili iliyopita majibu ya Obama yamekuwa yakibadilika kutoka katika sera yake ya afya maarufu kama ‘Obamacare’ hadi kufikia suala la kushindwa kuijenga upya kimfumo Libya hasa baada ya kumuua Rais wa nchi hiyo Moammar Gadhafi Oktoba, 2011.
Katika mahojiano aliyoyafanya na Agosti, 2014 na gazeti la New York Times, Obama alitetea uamuzi wa Marekani pamoja na washirika wake kumuondoa Gadhafi madarakani akifafanua kuwa lilikuwa jambo muhimu kufanyika. Katika maelezo hayo alisema pia kuwa kama wasingeshiriki oparesheni hiyo Libya ingekuwa kama Syria.
Katika mahojiano hayo hayo pia alisema “nadhani sisi na wenzetu wa Ulaya hatukuweka mkakati mzuri hasa katika suala la ujenzi wa Libya mpya baada ya Gadhafi kufariki.
Hili ni somo ambalo nimelipata na nimekuwa nikilitumia kila inapotokea hoja ya kutuhitaji kuingilia migogoro kivita. Pia swali kuhusu wajibu baada ya kutumia mbinu hiyo,” anasema Obama.
Lakini tena katika hotuba yake katika Umoja wa Mataifa Septemba, 2015 ambapo pia alisema uamuzi wa kuivamia Libya ulikuwa sahihi maana ulisaidia maafa makubwa kutotokea kwa kuwa Gadhafi alikuwa kaamua kuangamiza wananchi wote wa mji wa Benghazi.
Obama alikiri katika hotuba yake hiyo ya Umoja wa Mataifa kwa kusema; “japokuwa tuliwasaidia wananchi wa Libya na kuwaondolea udikteta, umoja wetu ulipaswa kufanya zaidi na hasa katika kuziba mianya tuliyokuwa tumeikuta na ile tuliyoitengeneza.
Marekani na washirika wake ni lazima tukubali kushiriki shughuli hizi kwa umakini zaidi siku zijazo kama Jumuiya ya Kimataifa na hasa kujengea uwezo nchi ambazo ziko kwenye dhiki ili zisiangamie kabisa.
Wachambuzi wa masuala haya wanasema kauli hii inatokana na kitendo cha Rais Obama kumpinga mara kwa mara mtangulizi wake rais Bush hasa alivyoshindwa kumudu kuisimamia Iraq baada ya kuuangusha utawala wa Sadam Hussein.
Lakini mwezi Aprili, 2016 Obama alibadili tena kauli yake kuhusu kukiri kushindwa Libya na akatoa lawama zaidi kuwa waliofanya jambo hilo kuwa hivyo ni washirika wao katika hasa Uingereza na Ufaransa.
“Kila nikifikiria na kujiuliza nini kilienda vibaya naona ipo haja ya kujadiliwa. Niliwaamini wenzetu wa Ulaya na sababu kubwa ilikuwa ukaribu wa nchi zao na Libya.
Kwa hiyo niliwategemea sana katika kufatilia mambo kule,” alisema na kisha kufafanua kuwa Rais wa Ufaransa wakati huo Nicolas Sarkozy alipoteza nafasi yake katika uchaguzi uliofanyika mwaka mmoja baada ya uvamizi Libya na pia akasema Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron naye akajikuta anakabiliwa na masuala mengi.
Jambo lingine linalojadiliwa na tukio la mwaka 2013 ambapo Marekani haikutumia majeshi katika kukabiliana na matumizi ya silaha za kikemikali nchini Syria. Msaidizi mmoja wa Obama anasema kuwa, kitendo cha kutumia majeshi kingesababisha machafuko makubwa zaidi hasa katika miji iliyokuwa chini ya Rais wa nchi hiyo Bashar Assad.
Anasema kitendo hicho kingeongeza vifo vya watu hata kuliko 470,000 ambao wamekufa kutokana na vita ndani ya Syria. “Kumvamia Assad bila kuwa na mkakati wa namna ya kuziba nafasi yake kweli ingesaidia kumng’oa na kisha ingewezekana kabisa kuiacha Syria nzima ikiwa chini ya ISIS.
Kitendo hiki kingeziweka pabaya nchi rafiki kwa Marekani mfano Uturuki na Jordan pamoja na Iraq. Na jambo hili lingeiweka Marekani katika mgogoro mkubwa zaidi.
Pia inaelezwa kuwa kitendo cha Obama kukataa kuisaidia silaha za kujilinda nchi ya Ukraine ili kukabiliana na majeshi yaliyokuwa yakiiunga mkono Urusi mashariki mwa nchi hiyo, nacho kinaingizwa katika orodha hii.
Kwa mujibu wa chanzo cha taarifa hii, Obama hakukubaliana na mpango huo kwani kama ingelitokea silaha za Kimarekani kumuua mwanajeshi wa Urusi basi kungeibuka mgogoro mkubwa mno.
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment