‘NI vita’, hivyo ndivyo tafsiri inapatikana kufuatia mvutano mkali
ulioibuka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kati ya
Mchungaji Peter Msigwa na Patrick Ole Sosopi ambao wanapambana kuwania
nafasi ya uenyekiti kanda ya Nyasa, RAI linachambua.
Msigwa ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini anapamba na Ole Sosopi ambaye
ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), kuwania
Kanda hiyo ya Nyanda za Juu Kusini (Nyasa) inayojumuisha mikoa ya
Iringa, Mbeya, Rukwa, Njombe na Songwe.
Tangu maandalizi ya uchaguzi kanda nane za Chadema yalipoanza mwezi
uliopita kumekuwapo na majibizano kati ya wafuasi wa wagombea hao wawili
ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii
kuanika madhaifu ya kila mgombea.
Hata hivyo, Msigwa ameonekana kushambuliwa zaidi kutokana na madai
mbalimbali ikiwamo tabia ya kutoshirikiana na wabunge wenzake katika
kukijenga chama, pia kujiweka mbali na wabunge wa chama hicho kipindi
walipokuwa wakipambana kutetea madai yao kwa Naibu Spika wa Bunge Dk.
Tulia Ackson.
Aidha, taarifa zilizolifikia RAI zinaeleza kuwa baadhi ya wabunge na
viongozi wa chama hicho wameonekana kusita kumuunga mkono Mbunge huyo
kutokana na madai ya ubinafsi aliouonyesha katika kipindi cha kampeni za
uchaguzi kwa kushindwa kushirikiana na makada wa chama hicho kuzunguka
sehemu mbalimbali.
“Pamoja na kuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 10, ameshindwa
kukisaidia chama chake kuongeza mbunge mwingine katika mkoa wa Iringa,
na pia haoneshi ushirikiano na wabunge wenzake pindi kunapotokea msimamo
fulani kwa masilahi ya chama,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo baadhi wafuasi wa Ole Sosopi walionekana kulalamika
kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo mmoja wao alisema:
“Nimeshangaa sana watu kunifuata inbox na kunitukana hata wengine
kutumia lugha ambayo si njema. Kumuunga mkono Ssosopi ‘it’s just my
perception.’ Kwa kuwa nina akili timamu siwezi kujibu matusi kama
mlivyofanya.
“Imeniuma sana, nimeumia sana. Naomba niliweke wazi hili, Peter Msigwa ni Mbunge wangu, ni mlezi wangu na sina ugomvi naye.
Sosopi na Msigwa wote ni Chadema na wote ni familia moja ndani ya chama
chetu Chadema,” aliandika Kumbusho Kagine katika ukurasa wake wa
Facebook.
Aidha, ili kupata sababu ya mvutano huo ambao umeibua madai
mbalimbali dhidi ya Msigwa, RAI lilimtafuta Mchungaji Msigwa ambaye
kwanza alisema yupo Mombasa nchini Kenya.
Pamoja na mambo mengine alisema hafahamu madai na tuhuma
alizoshushiwa na baadhi ya wafuasi wa mpinzani wake, na kuongeza kuwa
yeye si mtu wa kulinganishwa na Ole Sosopi.
“Hivi kwako unaona ni habari ya maana sana hii? Hivyo ni vitu vidogo
kwa kawaida huwa sipendi kupoteza muda na watu wenye akili ndogo
wanaweza kukupotezea muda,” alisema Msigwa.
Hata hivyo baadhi ya Wabunge waliodaiwa kutomuunga mkono Msigwa nl
James Milya – Mbunge wa Simanjiro ambaye alisema suala la mvutano huo
halitakiwi kuzungumzwa nje bali ni ndani ya chama.
Aidha, kwa upande wake Ole Sosopi alisema hawezi kuzungumzia madai
yoyote yanayotolewa dhidi yake kwa sababu taratibu za chama haziruhusu
kufanya kampeni.
Alisena: “Kwa sababu hata hao wanaojiita wafuasi wangu, sijawatuma,
wala sijatumia jukwaa lolote kuomba support yao ndio maana nasita
kuzungumzia chochote wanachokisema. Kwa sababu kwanza hata siwaamini
kweli kwamba wapo upande wangu ama la.”
Uchaguzi wa kanda ya Nyasa unatarajiwa kufanyika Desemba 22 mwezi huu mjini Tunduma mkoani Mbeya.
No comments:
Post a Comment