Waziri Mkuu wa New Zealand John Key ametangaza kwamba atajiuzulu wadhifa wake baada ya kuhudumu kwa miaka minane, akitaja sababu za kifamilia.
Alisema huo ndio uamuzi mgumu zaidi ambao amewahi kuufanya maishani.
"Sijui nitafanya nini baada ya hapa," alisema.
Bw Key, kiongozi anayependwa sana na watu, alikanusha taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba mkewe wa miaka 32 alikuwa amempa makataa.
Aidha, alisema hatawania muhula wa nne uchaguzi mkuu utakapofanyika mwaka 2017.
Makamu Waziri Mkuu Bill English anatarajiwa kuchukua majukumu ya uwaziri mkuu hadi chama cha National Party kikutane na kumteua waziri mkuu mpya.
Bw Key alitangaza kujiuzulu kwake kwenye kikao cha wanahabari cha kila wiki, ambapo alisema uamuzi wake umetokana na sababu za kinyumbani.
Alisema atang'atuka rasmi tarehe 12 Desemba.
Alisema kazi yake huhitaji kujinyima mambo mengi "kutoka kwa watu walio karibu sana nami" na kwamba watoto wake walikuwa "wameingiliwa sana".
"Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba nilijitolea kwa kila kitu. Sikuacha chochote kwenye tangi."
Akimrejelea mkewe Bronagh, aliambia kipindi cha habari cha Newstalk: "Tulizungumzia hili na anafurahishwa na wazo langu kuwa nyumbani zaidi lakini hakukuwa na makataa."
Bw Key, ambaye zamani alifanya kazi Merrill Lynch kama mfanyabiashara wa sarafu za kigeni, alifikisha kikomo utawala wa Chama ch leba mwaka 2008 alipomshinda Helen Clark.
Alichaguliwa kwa muhula wa tatu kupitia chama cha National Party Septemba 2014.
No comments:
Post a Comment