JK NA LOWASSA USO KWA USO KWENYE MAZISHI YA MEYA DAR.
WAMEKUTANA ndivyo unaweza kusema. Hatimaye mazishi ya kuuaga mwili wa
Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi,
yamewakutanisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Rais mstaafu wa
awamu ya nne, Jakaya Kikwete kwa kusalimiana na kushikana mikono.
Tukio hilo la aina yake liliwafanya watu mbalimbali waliokuwa katika
msiba huo kubaki wakishangaa, hasa baada ya Rais mstaafu Kikwete
kumfuata Lowassa na kumwuliza hali rafiki yake huyo wa zamani waliokulia
wote CCM.
Tangu wakati huo viongozi hao ambao walikuwa marafiki wa karibu tangu
ujana wao walikuwa wakirushiana vijembe ambapo jana walikutana ana kwa
ana katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wakati wa kuuaga
mwili wa Dk. Masaburi kabla ya kwenda kuzikwa nyumbani kwake Chanika
Manispaa ya Ilala.
Akiwa katika viwanja hivyo, Kikwete alipomwona Lowassa akiingia
viwanjani hapo alinyanyuka na kumfuta Lowassa katika kiti chake kisha
kusalimiana naye kwa kupeana mikoni huku wakizungumza.
Lowassa aliyekuwa ameketi jirani na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana pamoja na mkewe Regina Lowassa, alisimama na kumjibu salamu.
MTANZANIA ilimtafuta Lowassa na kutaka kujua alichozungumza na Rais
mstaafu Jakaya Kikwete ambapo alisema. “Ni kweli nimesalimiana na Jakaya
amenisalimia Assalam Aleykum nami nikamjibu. Kisha akaniuliza hujambo
nikamjibu sijambo. Nami nikamuliiza je nawe hujambo akasema hajambo basi
kila mmoja akaendelea na shughuli iliyotupeleka ya msiba,” alisema
Lowassa.
Kwa muda mrefu wanasiasa hao ambao wamewahi kuwa marafiki hadi kupewa
jina la utani ‘Boys II Men’, waliingia katika uhasama kwa kile
kinachodaiwa ni kusalitiana kisiasa.
Urafiki wa wawili hao ulianza kuingia doa mwaka 2008 wakati wa kashfa
ya Richmond iliyosababisha Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu kwa kile
alichoeleza ni kunyimwa haki ya kusikilizwa baada ya kuibuka kwa kashfa
hiyo kwa kile alichodai ilikuwa ni vita ya kutaka ‘uwaziri mkuu’.
Ukaribu wa Lowassa na Kikwete uliendelea kupungua na kuwa shakani
zaidi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana baada ya Lowassa kukatwa
jina lake katika kinyang’ anyiro cha kuwania nafasi ya kugombea urais
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuamua kuhamia Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema).
Kwa takribani mwaka mmoja sasa tangu mchakato wa ndani wa CCM wa
kumpata mgombea wake wa urais Julai 10, mwaka jana umalizike wawili hao
hawajawahi kukutana hadharani na kupeana mikono.
Katika mchakato huo Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi usiku wa
manane iliibuka na jibu kwamba, jina la Edward Lowassa limekatwa katika
watu wanaowania urais kupitia chama hicho.
Waliopitishwa na kuingia tano bora na Kamati Kuu walikuwa ni Bernard
Membe, Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina
Salum Ali, huku makada wengine 33 wakitupwa akiwamo Lowassa.
Kutokana na hali hiyo Lowassa alichukua aumuzi mzito wa kuihama CCM,
Julai 28, mwaka jana na kujiunga na Chadema na hatimaye kuteuliwa kuwa
mgombea urais kupitia chama hicho cha upinzani akiungwa mkoano na vyama
vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
JPM na familia ya Masaburi
Katika hali ya kushangaza msiba huo uligeuka kuwa furaha kwa
waombolezaji kutokana na maneno yaliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli
baada ya kupewa nafasi ya kutoa neno la pole kwa familia ya Masaburi.
Ule usemi wa msibani hakuna kupigiwa makofi jana ulibadilika baada ya
Rais Magufuli kufichua kile kilichofichwa na mdogo wa marehemu, Fowe
Masaburi, wakati akisoma wasifu wa marehemu kaka yake.
Katika wasifu huo Fowe alisema marehemu alifunga ndoa na Janeth
Masaburi na kwamba ameacha watoto 20 na wajane ambao hakutaja idadi yao.
Licha ya Rais Magufuli pia waombolezaji walionekana kushangaa kitendo
hicho kwani baada ya kusoma kipengele hicho iliibuka minong’ono
iliyodumu kwa dakika kadhaa kabla ya mshereheshaji kuwatuliza
waombolezaji kwa kuwataka wanyamaze.
Kutokana na kitendo hicho Rais Magufuli alianza kutoa neno lake kwa
kusema kwamba licha ya kutajwa mke mmoja kwenye wasifu yeye anafahamu
kuwa marehemu alikuwa na wake zaidi ya wanne hadi watano.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli ilisababisha waombolezaji wapige makofi
huku wengine wakiangua kicheko na baadhi walisikika wakisema ‘amekata
mzizi wa fitina’.
“Nimesikia kwenye wasifu kuwa marehemu alikuwa na mke mmoja lakini
mimi nafahamu alikuwa na wake zake ni wanne hadi watano. Kwa familia
zetu za Afrika kuwa na wake zaidi ya mmoja ni jambo la kawaida na hata
Mfalme Sulemani alikuwa na wake 1000 na ameandikwa kwenye vitabu vyote
vya dini,” alisema Rais Magufuli huku waombolezaji wakimpigia makofi na
kuangua vicheko.
“Nawapa pole wake wote wa marehemu pamoja na watoto wote hapa wametajwa 20 lakini nafahamu wanaweza kuwa zaidi ya hao,”.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli alitoa wito kwa familia hiyo
kutomkaribisha shetani ndani ya familia kwa kuhakikisha hawafarakani.
“Nitoe wito kwa wanafamilia hususani watoto baba yenu aliwapenda wote
bila kuwabagua na ndio maana alichagua kuzikwa sehemu ya wote.
“Mtoto mkubwa aliyezaliwa wa kwanza na marehemu ajue yeye ndiye
kiongozi wa familia na mjue mkishikamana ninyi hata mama zenu
watashikamana pamoja na ndugu wengine,” alisema Rais Magufuli.
Akimwelezea Dk. Masaburi alisema alimfahamu kama rafiki, ndugu na
mpiganaji wa CCM na kwamba historia yake haiwezi kufutika hususani
katika historia ya jiji la Dar es Salaam.
“Alikuwa ni mtu wa watu na umati huu ni ushahidi tosha kwamba
atakumbukwa na wengi katika historia yake kutokana na upendo na mambo
aliyowafanyia watu,” alisema Rais Magufuli.
VIONGOZI WALIOHUDHURIA
Mbali na Rais Magufuli, Lowassa na Rais mstaafu Kikwete viongozi
wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais Mstaafu, Dk. Mohamed Gharib
Bilal, Spika Mstaafu Anne Makinda, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John
Kijazi pamoja na wabunge na mawaziri.
Wengine ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu WASIFU WA MAREHEMU
Dk. Masaburi alizaliwa Machi 24 mwaka 1960 na alisoma Shule ya Msingi
Nseke iliyopo Serengeti na mwaka 1978 alijiunga na Sekondari ya
Wavulana ya Tabora na kuhitimu mwaka 1981.
Mwaka 1982 Dk. Masaburi alijiunga na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
(NIT) na kuhitimu mwaka 1985 na kupata cheti cha ufundi wa magari.
Mwaka 1985-1990 alichukua mafunzo ya ugavi na kupata Shahada ya
Ununuzi na Ugavi kutoka Bodi ya Ugavi wakati huohuo akichukua mafunzo
ya ununuzi na ugavi nchini Uingereza Chuo cha Chartered Institute of
Purchasing and Supply ambapo alitunikiwa cheti cha Diploma ya juu ya
Ununuzi na Ughavi mwaka 1988.
No comments:
Post a Comment