Kesi ya Akina Kitilya yatakiwa kuharakiswa!!!
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewataka mawakili wa Serikali
kuharakisha upelelezi wa kesi inayomkabili Kamishna Mkuu wa zamani wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitlya na wenzake.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Syprian Mkeha,
upande wa Serikali ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu,
Mutalemwa Kishenyi, wakati utetezi ukisimamiwa na Alex Mgongolwa.
Kishenyi alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo aliomba mahakama iahirishe shauri hilo.
“Mheshimiwa leo (jana) kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa pia
tumepokea maombi kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwa iahirishwe
kwa kuwa Takukuru nao hawajakamilisha upelelezi wao,” alisema Kishenyi.
Upande wa utetezi ulilalamika na kudai kwamba kesi bado ipo gizani
kwa sababu kila inapotajwa Serikali wanasema upelelezi haujakamilika.
“Ni takribani miezi sita sasa wateja wangu wapo mahabusu, naomba mawakili wa Serikali waharakishe suala hili,” alidai Mgongolwa.
Kutokana na hoja hiyo, mahakama ilipanga kesi hiyo itajwe tena Novemba 4, mwaka huu na washtakiwa walirejeshwa tena mahabusu.
Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa
Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na aliyekuwa Mwanasheria wa Benki
ya Stanbic, Sioi Solomon ambao wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali
likiwemo la utakatishaji wa fedha.
Mashtaka mengine ni kutumia nyaraka za kughushi na za uongo na
kujipatia isivyo halali Dola milioni sita za Marekani sawa na Sh bilioni
12, pia katika tarehe tofauti kati ya Agosti, 2012 na Machi, 2013
jijini Dar es Salaam washtakiwa walipanga kwa ushirikiano na watu
wengine kujipatia fedha kutoka serikalini kwa njia ya udanganyifu.
Pia ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Ofisi
za Makao Makuu ya Stanbic Tanzania Limited zilizopo Kinondoni, Shose
akiwa na nia ovu alighushi taarifa za maombi ya fedha katika Benki ya
Standard.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mbele ya mahakama hiyo Aprili, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment