SIRI ya kutenguliwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Bernard Mchomvu na bodi nzima ya wakurugenzi
imeelezwa kuwa ni kutokana na kushindwa kutimiza malengo ya Serikali ya
kukusanya mapato ya kutosha.
Chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya TRA kiliiambia MTANZANIA
kuwa huenda Bodi hiyo imeshindwa kubuni mikakati madhubuti ya kukusa
mapato tofauti na matarajio ya Serikali ya Dk. John Magufuli ya
kuhakikisha nchi inajitegemea kupitia vyanzo na mapato yake ya ndani.
Pia hatua hiyo ya Rais kutengua Bodi hiyo imechukuliwa siku chache
tangu itolewe ripoti ya hali ya uchumi ya Septemba mwaka huu ambayo ni
robo ya kwanza ya mwaka wa bajeti wa 2016/2017.
Taarifa nyingine zinadai huenda Bodi hiyo imetumbuliwa baada ya kutoa
mapendekezo mbalimbali juu ya utozaji wa kodi kwenye mizigo nje ya nchi
(on transit) pamoja na tozo za mipakani jambo ambalo uongozi wa juu wa
serikali umeona ushauri huo hautekelezeki.
Mapendekezo ya Bodi hiyo yalieleza kuwa kodi hizo zimekuwa zikichangia kushuka kwa uchumi wa nchi.
Taarifa ya Rais iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Gerson Msigwa, Ikulu jana, ilisema
uteuzi wa mwenyekiti mpya na bodi hiyo utatangazwa baadaye.
Hata hivyo taarifa hiyo ya Ikulu haikutaja sababu za kutenguliwa Bodi hiyo ya TRA.
Taarifa hizo zinadai kuwa kuhusu tozo inayojulikana kama “on transit
VAT”, bodi hiyo ilipendekeza iondolewe na badala yake uwekwe utaratibu
mzuri wa kuyabaini magari ambayo kweli yanatoka Bandari ya Dar es Salaam
kwenda nchi za Maziwa Makuu kuepuka udanganyifu unaoweza kujitokeza.
Ilidaiwa kwamba Bodi hiyo ilipendekeza pia uwekwe utaratibu mzuri
utakaowezesha mfumo wa kukusanya mapato ya mipakani ufanyike haraka
kuepuka ucheleweshaji usio na msingi kwa wafanyabiashara wa nje.
Chanzo hicho kilidai kuwa licha ya mchanganuo na ushauri huo, Serikali haikukubaliana na ushauri huo Bodi.
“Inawezekana ushauri huo haukukubaliwa na ilionyesha uongozi wote wa
Bodi umeshindwa kazi na hauwezi kwenda na kasi ya serikali ya sasa.
Ingawa Rais Magufuli alitoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutumia Bandari ya Dar es Salaam
bila tozo mbalimbali, bado wafanyabiashara hao hawakuchangamkia ofa hiyo
na wameendelea kutumia bandari nyingine zikiwamo Beira, Msumbiji na
Mombasa, Kenya.
Taarifa nyingine zinaeleza kuwa huenda pia Ikulu imechukua uamuzi huo
kwa kutoridhishwa na mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ambayo
yanaonekana kushuka.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Malipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Richard Kayombo, hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwa vile
simu yake iliita bila kupokewa.
IKULU YAKANA
Alipoulizwa kuhusu sababu za Rais kutengua uteuzi wa mwenyekiti na
kuvunja Bodi nzima ya TRA, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson
Msigwa alisema hajui sababu za uamuzi huo.
“Mimi ninachojua ni kwamba Rais ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa
Bodi ya TRA na wajumbe wake, lakini hizo sababu nyingine unazoniambia
kawaulize hao waliokupa taarifa hizo.
“Unajua siku hizi mtu anaweza kuamua kuandika kwenye mtandao kwamba
Msigwa kafa wakati si kweli, mimi sina taarifa nyingine zaidi ya hiyo,”
alisema Msigwa.
Ripoti ya BoT
Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliyotolewa Oktoba mwaka huu
inaonyesha kwamba makusanyo ya mapato ya ndani ya Septemba yalishuka kwa
asilimia 16.
Inaeleza kuwa Sh trilioni 1.4 au asilimia 84 ya lengo katika kipindi hicho, zilikusanywa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapato yaliyokusanywa na Serikali Kuu yalikuwa ni Sh trilioni 1.3 ambazo ni asilimia 84.3 ya lengo.
Ilieleza kuwa mapato yaliyotarajiwa kukusanywa na serikali za mitaa
kwa mwezi huo yalikuwa ni Sh bilioni 55.5 hata hivyo zilizokusanywa ni
Sh bilioni 41.2 pekee.
Ripoti hiyo inaonyesha mapato yasiyokuwa ya kodi yaliyokusanywa
katika kipindi hicho ni Sh bilioni 82.2 tofauti na lengo la Sh bilioni
225.7.
Vilevile, makusanyo ya kodi ya mapato yalishuka kwa asilimia 10 ya lengo la Sh bilioni 573.6.
Fedha za miradi kutoka nje zilizopatikana kwa kipindi hicho ni Sh bilioni 100.6 tofauti na lengo la Sh bilioni 993.6.
Ripoti ya BoT ya hivi karibuni inaonyesha kiwango cha makusanyo ya
mapato ya serikali katika kipindi hicho yameshuka na hivyo kusababisha
ukosefu wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.
Taarifa ya kushuka huko kwa makusanyo ya kodi, inaonyesha wazi kuwa imeishtua mamlaka za juu na sasa imeanza kuifanyia kazi.
Katika hatua hiyo, TRA imeanzisha oparesheni maalumu ya ukusanyaji kodi ambayo inakwenda hadi usiku.
Maofisa wake huenda katika maeneo mbalimbali hususan kwenye majengo
marefu, maeneo ya sinema na starehe nyingine kwa ajili ya kufanya
ukaguzi.
Gazeti dada la MTANZANIA, Mtanzania Jumapili, juzi liliwashuhudia
baadhi ya maofisa wa TRA wakiwa katika jengo la Dar Free Market kufanya
ukaguzi huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi.
Wakati huo huo, Dk. Magufuli jana alimteua Charles
Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA kujaza nafasi hiyo iliyokuwa
wazi kwa zaidi ya mwaka mmoja. Taarifa ya Ikulu iliyosainiwa na Msigwa
ilisema uteuzi huo unaanza mara moja.
No comments:
Post a Comment