Rais Mstaafu wa Tanzania Dkt Ali Hassan Mwinyi amesema amefurahishwa na utenda kazi wa Rais John Magufuli katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho amekuwa uongozini.
Dkt Mwinyi amesema kiongozi huyo wa sasa amepiga hatua sana katika kupambana na rushwa.
"Rushwa ilikuwepo tangu enzi ya Hayati Mwalimu Nyerere, aliipondaponda kabisa lakini hakuimaliza, na sote tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake," alisema Dkt Mwinyi baada ya kukutana na Dkt Magufuli katika ikulu ya Dar es Salaam Jumatano.
"Lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta Sunami, nafurahi sana."
Amesema kiongozi huyo amepiga hatua sana pia katika kuimarisha utendaji kazi Serikalini.
"Tusiwaache watu wakapata nafasi ya kuongea uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake na lengo lake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi aliyoifanya mwenzetu ni nzuri nzuri nzuri ya ajabu," alisema, kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.
Dkt Mwinyi, 91, aliongoza Tanzania kati ya 1985 na 1995.
No comments:
Post a Comment