MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameibua tena gumzo kubwa
katika vyombo vya habari na mitandao ya jami baada ya ukimya mrefu –
hususan tangu sakata lile la ‘kumchongea’ hadharani, mbele ya Rais John
Magufuli, aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe,
kuhusu ufisadi.
Kama vile katika suala la Kabwe, safari hii ni kuhusu ‘kuchongewa’
kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Simon
Sirro. Lakini tofauti mara hii ni kwamba ilikuwa ni mbele ya Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa.
Sakata lilianza Jumatano iliyopita katika hafla ya uzinduzi wa kituo
cha uboreshaji wa umeme wa uhakika jijini Dar es Salaam pale aliposema
kwamba kulikuwa na kikundi cha watu 10 kilichofika ofisini kwake na
kumshawishi apokee ‘hongo’ ya sh milioni tano kila mwezi kutoka kwa kila
mmoja, ili asizuie biashara ya shisha.
Kwanza kabisa, kabla sijaendelea nimekuwa nashangazwa sana hili suala
la uvutaji shisha kuibuka ghafla na kuonekana kama janga kubwa katika
jamii, pengine sawasawa na lile la dawa za kulevya ambalo sote twajua
jinsi linavyoharibu vijana wetu.
Mimi nadhani hadi miezi sita hivi iliyopita, ni Watanzania wachache
sana walikuwa wamewahi hata kusikia neno ‘shisha’ – achilia mbali kwamba
inadaiwa kuwa ni aina moja ya kilevi.
Lakini hivi kweli suala la shisha litikise nchi namna hii? Kuna
wangapi katika jamii tayari wameshaathirika na matumizi ya shisha?
Jamani kuna masuala mengi yanayohitaji kufuatiliwa katika kuboresha
maisha ya mamilioni ya Watanzania ambayo sasa hivi yako katika hali
mbaya kifedha.
Turudi kwenye mada. Mimi naamini – kutokana na jinsi Makonda
alivyokuwa anatoa kauli ile mbele ya Waziri Mkuu kwa kujiamini – ya
kutaka kupewa mlungula lilikuwa la kweli, ila tu nashangaa kwa nini
hakuchukua hatua stahiki pale pale, badala ya kulalamika hadharani mbele
ya Waziri Mkuu.
Mtendaji kama Mkuu wa Mkoa (tena wa Dar es Salaam), ambaye pia ni
Mwenyekiti ya Kamati ya Ulinzi na Usalama, hakuwa na namna nyingine ya
kulishughulikia tukio hilo la jinai isipokuwa tu kutafuta hafla na
kulalamika hadharani?
Hivi kweli hakuwa na vinasa sauti/vinasa picha za video
vilivyofichika ofisini mwake? Inawezekana anavyo, na inawezekana
alilinasa tukio hilo na hivyo kuwa tayari kutoa kama kielelezo kwenye
vyombo husika kama ushahidi hapo baadaye.
Lakini bila shaka alitaka pia kuonekana na umma, kwamba anafanya kazi
– yaani ni mchapa kazi na ndiyo maana hakutaka kulishughulikia suala
hilo kimya kimya. Nani angejua?
Njia hii anayotumia Makonda katika kupambana na ufisadi haifai, ni ya
kujionyesha zaidi kuliko dhamira ya dhati, na haifai kabisa kuigwa na
wengine. Au anataka kutuambia kuwa haviamini vyombo vya sheria
vinavyoshughulikia masuala haya?
Na hili ndiyo limekuwa tatizo kubwa kwa watendaji wakuu wa utawala –
zaidi wanataka waonekane na umma wanafanya kazi – kuliko kufanya kazi
yenyewe kikamilifu, ili wananchi waone matokeo yake. Kwa tafsiri yoyote
ile, kumchongea mtu hadharani, sio utaratibu mzuri, hasa pale hajatoa
ushahidi na hakuna tofauti na Wabunge wale waliofungiwa vikao kwa kutoa
kauli ambazo hawakuthibitisha pale pale walipotakiwa kufanya hivyo.
Vita dhidi ya ufisadi nchini mwetu inapita katika mitihani mikubwa
sana – mingi ni ya kushangaza na kuibua maswali iwapo kweli tuna nia
thabiti ya kuondokana na kansa hiyo au ni yale yale ya wananchi
‘kumwagiwa changa la macho’ ili waone tu kwamba vita hiyo daima inapamba
moto.
Kuna matukio ya kashfa kadha na kubwa kubwa za ufisadi zilizoibuka
nchini katika miaka ya karibuni, kuliko hii ya jaribio la hongo la
shisha, lakini takriban yote hayo utawala umekuwa ukiyashghulikia kwa
kuchechemea au kunyamaza kimya kabisa.
Kashfa hizi ni pamoja na zile za EPA, ESCROW, utoroshaji wanyama hai
na utafunaji wa fedha za umma, hususan katika halmashauri. Kwa ujumla
hali hii iliifanya TAKUKURU kupoteza imani (credibility) kwa umma katika
suala zima la vita dhidi ya ufisadi, suala ambalo ndilo linaweza
kulihakikishia Taifa amani na utulivu uliokuwepo uendelee.
Kwa ujumla, ukichunguza kwa makini historia ya vita dhidi ya ufisadi
iliyokuwa ikiendeshwa na watawala hapa nchini kabla ya ujio wa Rais John
Magufuli, huwezi kuacha kugundua vita hiyo ilikuwa imejaa ukosefu wa
ari, unafiki, uwongo, ujanjaujanja, ghilba, kiini macho, upotoshaji,
mizengwe, dhihaka na kila aina ya sifa hasi utakayofikiria, na matokeo
yake ni kuongezeka, si kupungua kwa tatizo hilo.
Chukulia mfano wa ufisadi mkubwa wa kuchotwa fedha kutoka Benki Kuu
katika Akaunti ya Tegeta Escrow. Ufisadi huu ulifikia kilele mwishoni
mwa mwaka 2014, pale Bunge lilipotoa maazimio ya kutaka wahusika wakuu
wawajibishwe, baadhi yao wakamatwe na kufunguliwa mashitaka.
Hakuna kilichotokea, isipokuwa tu baadhi yao walijiuzulu, ingawa kuna
mmoja alifukuzwa kazi na mwingine aliyejiuzulu kwa shinikizo kubwa,
alirejeshwa katika wadhifa wake kwa madai ni ‘mchapa kazi.’
Sote pia twafahamu ufisadi hukwaza maendeleo ya nchi na kwa ujumla,
kutia umasikini wananchi. Lakini pia huweza hata kuleta uvunjifu wa
amani na hali ya utulivu. Athari hii pia imeandikwa, si mahala pengine,
bali katika sentensi ya kwanza kabisa ya utangulizi (preamble) ya Sheria
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB Act) ya mwaka 2007.
Hivyo sote wananchi twalifahamu hili, hususan watawala wetu,
waliotunga sheria hiyo. Lakini cha ajabu ni kwamba kila wanapofanya
vitendo vyao vya ufisadi unaosababisha mtikisiko na wananchi kuanza kuja
juu, na hata kuonyesha kutishia amani iliyopo (kama vile kutaka kufanya
maandamano nchi nzima nk), basi watawala hao hao, badala ya kuchukua
hatua thabiti ya kuwashughulikia mafisadi, basi huanza kuwatuliza
wananchi na kuwahamasisha wafanye ibada kuiombea nchi amani!
Ufisadi wafanye wao, kuwalinda mafisadi wawalinde wao, kutishia amani
watishie wao, halafu eti ibada ya amani tufanye sisi! Majanga!
No comments:
Post a Comment