Kiongozi wa muda mrefu nchini Gambia Yahya Jammeh amekubali kung'atuka na kuondoka nchini humo, rais anayetambuliwa na jamii ya kimataifa amesema.
Adama Barrow ametangaza hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter, baada ya mazungumzo ya saa kadha yaliyonuiwa kumshawishi Bw Jammeh kukubali matokeo ya uchaguzi.
Mataifa ya Afrika Magharibi yamewatuma wanajeshi Gambia na kutishia kumuondoa Jammeh madarakani kwa nguvu.
Bw Barrow amekuwa nchini Senegal kwa takriban wiki moja.
Aliapishwa kuwa rais mpya wa Gambia katika ubalozi wa Gambia mjini Dakar mnamo Alhamisi.
Ametambuliwa na jamii ya kimataifa kama kiongozi mpya wa Gambia.
Bw Jammeh alkuwa amepewa makataa ya kuondoka madarakani kufikia saa sita mchana la sivyo aondolewe kwa nguvu na wanajeshi wanaoungwa mkono na UMoja wa Mataifa.
Amekuwa akishauriana na Rais wa Guinea Alpha Conde na mwenzake wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz.
Muda rasmi wa Jammeh kuongoza kikatiba ulifikia kikomo Jumatano.
Hata hivyo, akiwa bado rais, alifanikiwa kuhakikisha bunge linapitisha sheria ya kumruhusu kuendelea kutawala hadi Mei.
Kwa kuwa Bw Barrow tayari ameapishwa, taifa hilo ni kana kwamba lilikuwa na marais wawili kwa wakati mmoja.
Wanajeshi wa Ecowas kutoka Senegal na nchi nyingine za Afrika Magharibi waliingia nchini humo baada ya kuapishwa kwa Bw Barrow na walisema hawakukumbana na upinzani wowote.
Mbona Jammeh hataki kuondoka madarakani?
Bw Jammeh awali alikubali kwamba Bw Barrow alishinda uchaguzi lakini baadaye akabadili msimamo wake na kusema hangeachia madaraka.
Alitangaza hali ya tahadhari ya siku 90 na kuhimiza "amani, utulivu na kufuatwa kwa sheria" baada ya kile alichosema ni udanganyifu uchaguzini.
Alisema tume ya uchaguzi ilifanya makosa mengi, na baadhi ya wafuasi wake walizuiwa kupiga kura vituoni.
Tume hiyo baadaye ilikubali kwamba baadhi ya matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na makosa, lakini ikasema makosa hayo hayangeathiri ushindi wa Bw Barrow.
Bw Jammeh amesema atasalia madarakani hadi uchaguzi mpya ufanyike.
Hatua yake ya kuendelea kung'ang'ania madaraka itahakikisha kwamba hashtakiwi kutokana na makosa aliyoyatenda wakati wa utawala wake.
Mbona Senegal inaongoza kumkabili
Ecowas, Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, iliipa Senegal jukumu hilo kwa sababu taifa hilo linaizunguka Gambia.
Kanali Abdou Ndiaye, msemaji wa jeshi la Senegal, amesema Ecowas iliamua kumuwekea Jammeh makataa ili kujaribu kupata suluhu ya kidiplomasia.
Hii inaifanya vigumu kufikiria ni vipi wanaweza kuwashinda wanajeshi wa kanda hiyo, anasema mwandishi wa BBC wa masuala ya usalama Afrika Tomi Oladipo.
Nigeria imetuma ndege za kivita na ndege nyingine za kawaida, pamoja na wanajeshi 200 nchini Senegal. Wanajeshi hao walienda Senegal Jumatano asubuhi.
Meli za kivita za Nigeria pia zimewekwa tayari baharini.
Manowari moja iliondoka Lagos Jumanne na itakuwa na jukumu la kuwaokoa raia wa Nigeria walio nchini Gambia.
Ghana pia inachangia wanajeshi.